Maana halisi ya falsafa ya 'Nitakuwa tayari kufungwa kwa ajili ya matatizo ya watu', au Falsafa ya Kufungwa, ni uvutano mkubwa uliopo kati ya Roho Mtakatifu na Roho wa Shetani kwa sisi wanadamu wote. Jambo lolote baya limtokealo mwanadamu husababishwa na Shetani na si Mungu na watu hupata matatizo kwa sababu ya kudharau miito ya mioyo yao wenyewe, au kudharau kile Roho Mtakatifu anachowambia. Unaweza kuvunja sheria kwa manufaa ya wengi kwani mibaraka haikosi maadui. Ukifungwa kwa kuvunja sheria kwa ajili ya manufaa ya wengi watu watakulaani lakini Mungu atakubariki. Kwa nguvu ya uwezo wa Roho Mtakatifu Mungu atamshinda Shetani kwa niaba yako. Tukijifunza namna ya kuwasiliana na Roho Mtakatifu hatutapata matatizo kwani Mungu anataka tuishi kwa amani katika siku zote alizotupangia, licha ya damu yetu kuwa chafu. Mtu anapokufa kwa mfano, Roho wa Shetani amemshinda Roho Mtakatifu na Roho Mtakatifu hatalipendi hilo kwa niaba ya Mungu. Ikitokea mtu akayashinda majaribu ya Shetani katika kipindi ambacho watu wote wameyashindwa; mtu huyo amebarikiwa na Mungu, ili aitumie mibaraka hiyo kuwaepusha wenzake na roho mbaya wa Shetani. Nikisema 'Kwa nguvu ya uwezo wa Roho Mtakatifu Mungu atamshinda Shetani kwa niaba yako' namaanisha, Roho Mtakatifu ana uwezo wake na Roho wa Shetani ana uwezo wake pia. Ukimshinda Roho wa Shetani uwezo wa Roho Mtakatifu umekuwa mkubwa kuliko uwezo wa Roho wa Shetani, na ukishindwa kumtii Roho Mtakatifu uwezo wa Roho wa Shetani umekuwa mkubwa kuliko uwezo wa Roho Mtakatifu, ilhali uwezo wa Mungu ni mkubwa kuliko wa Roho Mtakatifu na wa Roho wa Shetani kwa pamoja. Mungu humtumia Roho Mtakatifu kumlindia watoto wake ambao ni sisi dhidi ya Shetani … Kila akifanyacho Roho Mtakatifu hapa duniani ni kwa niaba ya Mungu, na tukimtii Roho Mtakatifu Mungu atamshinda Shetani kwa niaba yetu. Mtu anapofungwa kwa kutetea maslahi ya umma wewe unayemfunga umemtii Roho wa Shetani. Yule anayefungwa amemtii Roho Mtakatifu maana amebarikiwa, na mibaraka haikosi maadui.
Enock Maregesi